JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
 
     
    SEKTA YA MIUNDO MBINU
 
[ Miundo Mbinu ] Programu.. [ Nyumbani ] au
 
Barabara

Mkoa wa Mwanza una barabara zenye jumla ya urefu wa km.5,598, katika hizo zimo barabara kuu zenye urefu wa km.397, barabara za mikoa zenye jumla ya km.1,087, barabara za Wilaya km.1,398.7 na km.2,715.4 barabara za vijijini.
Mtandao huu ni muhimu sana kwa wakazi zaidi ya milioni tatu na nusu wa mkoa huu katika kupata huduma mbalimbali za kijamii na unategemewa kuwasaidia wakazi hawa katika kukuza na kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara, kuendesha shughuli za uvuvi, uchimbaji wa madini, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.

 

pamoja na umuhimu wa barabara hizi ni 38%tu ndiyo ziko katika hali nzuri na asilimia 62 zinahitaji matengenezo makubwa.  Sababu  ya  kuwa  na  asilimi  kubwa  ya  barabara zinazohitaji matengenezo makubwa ni  pamoja  na  ufinyu  wa  bajeti  tunayotengewa  kwa  ajili  ya matengenezo. Wakati mwingine kutokana na mvua kubwa zinaponyesha, barabara zetu zinazidi kuwa na hali mbaya sana hivyo bajeti finyu inayotengwa kila mwaka husababisha zisifanyiwe matengenezo ya mara kwa mara.

Mkakati wa Kuboresha Barabara

Ili kukabiliana na hali hii mkoa umeamua ifuatavyo:-

1.Kuteua barabara zinazoongoza kwa umuhimu na kuona kuwa zinatengewa fedha za kutosha kuzikarabati, japo kwa awamu.
2.Kutumia wajumbe wa bodi ya barabara ya mkoa pamoja na wataalamu wahandisi tulionao kuona kunakuwa na thamani halisi ya fedha (Value for money) kulingana na matengenezo yatakayofanywa katika barabara zilizotengewa fedha. Hili ni sehemu ya maazimio ya kikao cha Bodi ya Mkoa ya barabara mwezi Machi mwaka huu.

 

 

Vivuko, Meli, Bandari na Magati

Vivuko na meli ni sehemu muhimu katika usafiri ndani ya mkoa wetu. Hali ya vivuko vyetu vyote vya serikali siyo vya kuridhisha, na vimekuwa vikisababisha hofu kwa watumiaji wake. Kidogo sasa kasi ya uundaji wa kivuko kipya pale Mwanza South Port kwa ajili ya kuvukia Kigongo-inaendelea vizuri na ni matarajio yetu kuwa kweli kitakuwa tayari wakati wowote kuanzia sasa. Hali ya MV clarius na Butiama, meli zinazosafirisha abira na mizigo baina ya Mwanza na Ukerewe pia siyo nzuri sana huku MV Serengeti ikiwa haifanyikazi. Kwa ujumla suala la udhibiti wa usalama wa vyombo vya majini linahitaji kutiliwa mkazo hata kwa vyombo vinavyomilikiwa na serikali. Kwa mantiki hiyo, kitengo cha SUMATRA kilichopo hapa Mwanza bado kina nafasi ya kufanya kazi nzuri zaidi. Pamoja na hali hiyo ya vivuko na meli, serikali mkoani na katika Wilaya zote zinazopakana na ziwa hazina hata boti kwa shughuli za utawala, ingawa 43% ya eneo la mkoa wa Mwanza ni maji (ziwa Victoria). Hali ya bandari zetu tulizonazo pia inahitaji kuboreshwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kina kinabakia cha kutosha kwa kuondoa mchanga (dredging) pale inapohitajika, na kufanya walau matengenezo yaliyo muhimu katika Bandari na Magati yetu.

pamoja na hayo, serikali mkoani Mwanza inaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Wizara ya miundombinu pale inapohitajika ili kuharakisha utatuzi wa matatizo ya sekta hii.      Mkoa wetu tuliomba fedha katika bajeti yetu ya mkoa ya mwaka 2007/2008 fedha kwa ajili ya ununuzi wa Boti mbili (2) moja kwa Wilaya ya Ukerewe na moja kwa Wilaya ya Sengerema kwa shughuli za utawala na doria ndani ya ziwa Victoria, lakini bahati mbaya fedha hiyo haikupatikana pamoja na umuhimu mkubwa uliopo kuzipata boti hizo. Bado tunaomba serikali ilipe uzito wa pekee suala hili kwani ni muhimu kwa Ulinzi na Usalama wa maeneo haya hasa katika Ziwa Victoria.

Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza

Pamoja na viwanja vya ndege kadhaa ndani ya mkoa vilivyochini ya TAA na vile vya makampuni binafsi, tuna uwanja wetu mkubwa wa ndege hapa Mwanza ambao unafanyiwa matengenezo na upanuzi. Jambo hili tunalipokea kwa furaha kwani upanuzi huo utatuweka katika nafasi nzuri zaidi kuelekea kwenye ndoto yetu ya kuifanya Mwanza kitovu cha biashara katika eneo hili la maziwa makuu.

 
 
 
[ Miundo Mbinu ] [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
© 2009 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa S.L.P 119 Mwanza, Simu:028-2501037/2500366,Fax: 0282501057;Email:info@mwanza.go.tz